KATIBA YA KIKUNDI CHA KUSAIDIANA WAKATI WA MISIBA

MAILINE CARRIERS LIMITED - STAFF WELFARE

SURA YA KWANZA: JINA, MAKAZI NA MALENGO

Kifungu cha 1: Jina la Kikundi

Kikundi kitaitwa MAILINE CARRIERS LIMITED – STAFF WELFARE (Kikundi cha Kusaidiana Wakati wa Misiba) (baadaye kitaitwa "Kikundi").

Kifungu cha 2: Makazi

Makazi makuu ya Kikundi yatakuwa kama yatakavyoamuliwa na Mkutano Mkuu wa wanachama.

Kifungu cha 3: Malengo ya Kikundi

Malengo makuu ya Kikundi (Staff Welfare) ni:

  1. Kusaidiana kifedha na kijamii wakati wa misiba.
  2. Kuimarisha mshikamano na umoja miongoni mwa wanachama.
  3. Kutoa msaada wa haraka na wa heshima wakati wa vifo vilivyobainishwa katika Katiba hii.

SURA YA PILI: UANACHAMA (STAFF WELFARE)

Kifungu cha 4: Sifa za Mwanachama
  1. Mwanachama atakuwa mtu aliyekubali na kusaini kuzingatia Katiba hii.
  2. Mwanachama atalipa ada na michango kama itakavyoamuliwa.
Kifungu cha 5: Haki za Mwanachama
  1. Kushiriki mikutano yote ya Kikundi.
  2. Kupiga kura na kuchaguliwa katika nafasi za uongozi.
  3. Kupata msaada wa Kikundi wakati wa msiba kulingana na Katiba hii.
Kifungu cha 6: Wajibu wa Mwanachama
  1. Kuhudhuria mikutano ya Kikundi.
  2. Kulipa ada na michango kwa wakati.
  3. Kuheshimu viongozi na wanachama wengine.
Kifungu cha 7: Kuacha Kazi/Kukoma Uanachama
  1. Uanachama wa Staff Welfare utakoma moja kwa moja pale mfanyakazi atakapoacha kazi katika MAILINE CARRIERS LIMITED kwa sababu yoyote ile (kujiuzulu, kufukuzwa, kustaafu au kumaliza mkataba).
  2. Mwanachama aliyeacha kazi hatakuwa na haki ya kuendelea kupata msaada au kushiriki maamuzi ya Kikundi.
  3. Fedha za ada au michango iliyokwisha lipwa hazitarejeshwa baada ya kukoma kwa uanachama.
  4. Endapo tukio la msiba limetokea wakati mwanachama bado yupo kazini na amekidhi masharti yote, atastahili msaada hata kama ataacha kazi kabla ya msaada kutolewa.
  5. Baraza la Uongozi litakuwa na mamlaka ya kuthibitisha rasmi kukoma kwa uanachama kwa mujibu wa kifungu hiki.

SURA YA TATU: MUUNDO WA UONGOZI

Kifungu cha 8: Baraza la Uongozi
  1. Kutakuwa na Baraza la Uongozi litakalosimamia na kuratibu shughuli zote za Kikundi.
  2. Baraza la Uongozi litakuwa na mamlaka ya mwisho ya kushughulikia na kuamua rufaa zote zinazohusu wanachama au viongozi wa Kikundi.
  3. Maamuzi ya Baraza la Uongozi yatakuwa ya mwisho na ya lazima kutekelezwa.
  4. Viongozi wote wa Kikundi watawajibika moja kwa moja kwa Baraza la Uongozi katika utekelezaji wa majukumu yao.
  5. Baraza la Uongozi litakuwa na mamlaka ya kuchukua hatua za kinidhamu kwa kiongozi yeyote atakayekiuka Katiba, kanuni au maamuzi ya Kikundi.
  6. Baraza la Uongozi litakutana mara kwa mara au kwa dharura pale itakapohitajika.
Kifungu cha 9: Vyeo vya Uongozi

Viongozi wa Kikundi watakuwa:

  1. Mwenyekiti
  2. Makamu Mwenyekiti
  3. Katibu Mkuu
  4. Naibu Katibu Mkuu
  5. Mweka Hazina
  6. Mweka Hazina Msaidizi

SURA YA NNE: MAJUKUMU YA VIONGOZI

Kifungu cha 10: Mwenyekiti
  1. Kuongoza mikutano yote ya Kikundi.
  2. Kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya Kikundi.
Kifungu cha 11: Makamu Mwenyekiti
  1. Kusaidia Mwenyekiti katika majukumu yake.
  2. Kaimu nafasi ya Mwenyekiti anapokosekana.
Kifungu cha 12: Katibu Mkuu
  1. Kuandaa na kuhifadhi kumbukumbu zote za Kikundi.
  2. Kuandika kumbukumbu za mikutano.
Kifungu cha 13: Naibu Katibu Mkuu
  1. Kusaidia Katibu Mkuu.
  2. Kaimu nafasi ya Katibu Mkuu anapokosekana.
Kifungu cha 14: Mweka Hazina
  1. Kusimamia fedha zote za Kikundi.
  2. Kuhifadhi kumbukumbu za mapato na matumizi.
Kifungu cha 15: Mweka Hazina Msaidizi
  1. Kusaidia Mweka Hazina.
  2. Kaimu nafasi ya Mweka Hazina anapokosekana.

SURA YA TANO: MAMBO YANAYOSTAHILI KUSAIDIWA

Kifungu cha 16: Aina za Misiba Inayosaidiwa

Kikundi kitatoa msaada katika misiba ifuatayo:

  1. Kifo cha mwanachama.
  2. Kifo cha mwenza (mume au mke) wa mwanachama, awe wa kiume au wa kike kwa mujibu wa ndoa au mahusiano yanayotambulika kisheria.
  3. Kifo cha mama au baba wa mwanachama.
  4. Kifo cha mtoto wa mwanachama.

Msaada utatolewa kwa mujibu wa taratibu na viwango vitakavyoamuliwa na Mkutano Mkuu.

SURA YA SITA: MASHARTI YA KUZINGATIWA

Kifungu cha 17: Masharti ya Jumla
  1. Mwanachama lazima awe amelipa ada zake kikamilifu ili kustahili msaada wa Kikundi.
  2. Mwanachama atakayekuwa na madeni ya ada ya zaidi ya miezi mitatu (3) hatastahili msaada hadi atakapokamilisha malipo.
  3. Msaada hautatolewa endapo taarifa ya msiba haitawasilishwa kwa maandishi kwa uongozi ndani ya siku saba (7) tangu kutokea kwa tukio.
  4. Tukio la msiba linalostahili msaada lazima lihusishe moja ya matukio yaliyobainishwa kwenye Katiba hii.
  5. Msaada hautatolewa kwa tukio lililotokea kabla ya mwanachama kujiunga au kabla ya kukamilisha ada zinazohitajika.
  6. Mwanachama atawajibika kutoa ushahidi wa tukio la msiba pale utakapohitajika (mfano: barua ya kifo au uthibitisho wa ndugu).
  7. Nidhamu, heshima na utii kwa Katiba, kanuni na maamuzi ya Kikundi ni sharti la msingi kwa kila mwanachama.
  8. Mwanachama au kiongozi atakayekiuka Katiba anaweza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa maamuzi ya Baraza la Uongozi.
Kifungu cha 18: Mwanachama Asipotimiza Masharti
  1. Mwanachama atakayeshindwa kutimiza masharti yaliyowekwa katika Katiba hii atapewa onyo la maandishi na Baraza la Uongozi.
  2. Endapo ataendelea kutokutimiza masharti baada ya onyo, anaweza kusimamishwa kwa muda au kunyimwa haki za uanachama hadi atakapokidhi masharti.
  3. Mwanachama anaweza kukosa kabisa haki ya kupata msaada kwa tukio husika endapo atabainika kukiuka masharti kwa makusudi.
  4. Maamuzi yote ya kinidhamu yatafanywa na Baraza la Uongozi na yatakuwa ya mwisho.

SURA YA SABA: FEDHA NA MICHANGO

Kifungu cha 19: Ada na Vyanzo vya Fedha
  1. Ada ya uanachama itakuwa Shilingi 10,000/= (Tsh elfu kumi) kwa kila mwezi kwa kila mwanachama.
  2. Mwanachama anaruhusiwa kulipa ada ya mwaka mzima kwa mkupuo (lump sum) kwa mwaka husika endapo atapenda.
  3. Michango yote ya wanachama, ikiwemo ada na michango maalum, itatumwa na kuhifadhiwa katika akaunti rasmi ya M-Koba ya Staff Welfare pekee na si mahali pengine popote.
  4. Hairuhusiwi kupokea au kuhifadhi fedha za Kikundi kupitia akaunti binafsi ya kiongozi au mwanachama yeyote.
  5. Vyanzo vingine vya fedha vitajumuisha:
    1. Michango maalum ya wanachama.
    2. Misaada halali kutoka kwa wadau wengine.
Kifungu cha 20: Matumizi ya Fedha
  1. Fedha zitatumika kwa madhumuni ya kusaidia misiba na shughuli za Kikundi pekee.

SURA YA NANE: MIKUTANO

Kifungu cha 21: Mkutano Mkuu
  1. Mkutano Mkuu ni chombo kikuu cha maamuzi.
  2. Utafanyika angalau mara moja kwa mwaka.
  3. Mikutano ya Kikundi itaitishwa na Mwenyekiti.
  4. Endapo Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti hawapo au wameshindwa kutekeleza wajibu wao, Katibu Mkuu atakuwa na mamlaka ya kuitisha kikao.
  5. Ikiwa pia Katibu Mkuu hayupo, Baraza la Uongozi linaweza kumteua mjumbe mmoja wa uongozi kwa maandishi kuitisha na kuongoza kikao hicho kwa muda.
Kifungu cha 22: Maamuzi ya Mikutano
  1. Maamuzi ya Mkutano Mkuu yatafanywa kwa kura ya theluthi mbili (2/3) ya wanachama waliopo kwenye kikao halali.

SURA YA TISA: MAREKEBISHO YA KATIBA

Kifungu cha 23: Marekebisho
  1. Katiba hii inaweza kurekebishwa kwa azimio la Mkutano Mkuu kwa kura ya theluthi mbili (2/3) ya wanachama waliopo.

SURA YA KUMI: KUVUNJWA KWA KIKUNDI

Kifungu cha 24: Kuvunjwa
  1. Kikundi kinaweza kuvunjwa kwa azimio la Mkutano Mkuu kwa kura ya theluthi mbili (2/3) ya wanachama wote.

Katiba hii imepitishwa na Mkutano Mkuu wa Kikundi siku ya ________ mwaka ________.

_______________________

Mwenyekiti

_______________________

Katibu Mkuu